MTOTO WA MKULIMA AANZA HOTUBA YAKE KWA WIMBO WA LUCKY DUBE KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA WALEMAVU WA NGOZI TANZANIA TAREHE 04 MEI 2010 VIWANJA VYA GARDEN MJINI IRINGA
Ndugu Wananchi,
 Wakati ninapoalikwa  kwenye Mikutano, Makongamano, Warsha na Maadhimisho ya Shughuli za  Walemavu wa Ngozi kama hii ya leo, huwa ninapata shida sana niseme nini  kwa Watanzania na Ulimwengu kwa ujumla. Hii inatokana na kuendelea  kuwepo kwa vitendo viovu vya ukatili yakiwemo Mauaji wanayofanyiwa Ndugu  zetu, Baba zetu, Mama zetu, Dada zetu na Kaka zetu wenye Ulemavu wa  Ngozi ambao tumezoea kuwaita Albino.
 Wakati wa Ubaguzi wa  Rangi Nchini Afrika Kusini, Mwanamuziki Mashuhuri Barani Afrika – Hayati  Lucky Dube aliimba Wimbo unaoitwa – “Different  Colours-One People” akiwa na maana ya Rangi  Tofauti, Binadamu Mmoja. Moja  ya Beti za Wimbo huu unasema:
“Different Colours/one  People
             Different Colours/one  People
             Hey you Government
             Never try to separate the  People
             Hey you Politician
             Never try to separate the  People
             They were created in the  Image of God
             And who are you to  separate them
             Bible says, He made Man  in His Image
             But it didn’t say Black  or White
             Look at me you see BLACK
             I look at you I see WHITE
             Now is the time to kick  that away”
KWA TAFSIRI YA KISWAHILI ISIYO RASMI HAYATI LUCKY DUBE ANAUAMBIA ULIMWENGU KUWA..
KWA TAFSIRI YA KISWAHILI ISIYO RASMI HAYATI LUCKY DUBE ANAUAMBIA ULIMWENGU KUWA..
“Rangi tofauti – Binadamu  Mmoja
              Rangi tofauti – Binadamu  Mmoja
              Nyie Serikali –  Msithubutu kubagua Watu
              Nyie Wanasiasa  –Msithubutu kubagua Watu
              Waliumbwa kwa Sura ya  Mungu
              Nyie ni kina nani  muwabague
              Biblia inasema: Mungu  alimuumba Mtu kwa Mfano wake
              Lakini hakusema Mweusi  au Mweupe
              Niangalie mimi unaniona  ni Mweusi
              Nikikuangalia naona  Mweupe
Nimeona nianze hotuba hii  na Wimbo huu wa Hayati Lucky Dube kwa sababu ulikuwa unapinga Ubaguzi  wa rangi waliofanyiwa Waafrika Weusi Nchini Afrika ya Kusini wakati wa  Utawala wa Makaburu.
 Leo hii, Karne ya Sayansi  na Teknolojia, Watanzania tunawabagua Walemavu wa Ngozi, tunawakata  viungo na kuwaua Ndugu zetu kwa imani za Kishirikina. Hii ni dhambi  ambayo hatutasamehewa kwa Mungu. Naomba Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu  wa Ngozi Tanzania usimame. Hivi huyu Bwana mbali na yeye kuwa Mweupe na  mimi Mweusi tuna tofauti gani nyingine? Mungu amemuumba kama mimi.  Kampa viungo vyote kama mimi. Sasa imani za Kijinga kuwa ukipata Kiungo  cha Albino utakuwa tajiri zinatoka wapi? 
 Kama ingekuwa hivyo, kwa  nini msiende Nchi za Ulaya na Asia kwa sababu Mabara hayo yana Watu  wengi wenye Ngozi Nyeupe ili muwe Matajiri. Nami leo nawaambia  Watanzania wote kwamba Mungu ametuumba sote kwa Mfano wake tuachane  na imani Potofu za Kishirikina.
 Ndugu Wananchi,
 Sera ya Taifa ya Walemavu  ya mwaka 2004, inaonyesha kuwa, Tanzania kuna Walemavu wa Viungo  wapatao takariban 3,456,900. Inasadikiwa kwamba, idadi hii ya Walemavu  inaweza ikawa ni kubwa zaidi kwa sasa. Aidha, Takwimu zinazotokana na  Sensa Ndogo iliyofanywa kwa haraka haraka mwaka 2007 kutokana na kutokea  mauaji ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi zinaonyesha kuwa Tanzania ina  Watu wenye Ulemavu wa Ngozi wapatao takriban 8,000. Takwimu hizi ambazo  zinahitaji kuhakikiwa zinatoa changamoto kwa Wadau mbalimbali kufanya  Sensa itakayotupa hali halisi ya Watu wenye Ulemavu Nchini ili Serikali  iweze kupanga mikakati madhubuti katika kuhudumia kundi hili muhimu  katika Jamii.
 Ndugu Wananchi,
 Ni kweli kwamba  tunaadhimisha Siku ya Walemavu wa Ngozi Tanzania wakati ambapo bado  tunayo Changamoto kubwa ya matukio ya mauaji ya Walemavu hawa Nchini.  Tangu Oktoba 2009 hadi sasa, Taarifa tulizonazo ni za Mauaji ya Mlemavu  Mmoja (1) wa Ngozi na Watatu (3) waliojeruhiwa. Hata hivyo, pamoja na  matukio hayo ya hivi karibuni; hali ya Mauaji ya Walemavu wa Ngozi  Nchini yanaonyesha kupungua ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitatu  iliyopita. Hali hii ni kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na  Serikali katika kukabiliana na tatizo hili.
 Juhudi za Serikali
 Ndugu Wananchi,
 Moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na  kuitisha Kura ya Maoni kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya Mapambano  dhidi ya Vitendo vya Ukatili kwa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Serikali  iliwataka Wananchi kutaja Watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na Mauaji  au kukata Viungo vya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi, wawataje Waganga wa  Jadi wanaohusika, Wauaji, Wauzaji wa Viungo na Wafanyabiashara  wanaotumia Viungo hivyo. 
 Zoezi la Kura ya Maoni lilifanyika kwa Mikoa yote  Tanzania Bara mwezi Machi 2009. Jumla ya Watu 97,736  walipigiwa Kura kuwa wanahusika na makosa mbalimbali yakiwemo ya Mauaji  ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Upelelezi wa kina unaendelea kuhusu  Watuhumiwa na wale wote ambao ushahidi unapatikana wanafikishwa  Mahakamani. Hadi sasa, Watu 3,217 wamefikishwa katika  Vituo vya Polisi, Watu 295 wamefikishwa Mahakamani na  Watu 106 wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwemo  ya Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Kati ya  kesi zilizofikishwa Mahakamani, 11 ni za mauaji ya  Walemavu wa Ngozi. Kesi tatu zimetolewa hukumu na  Watuhumiwa Wanane (8) wamehukumiwa kifo. Upelelezi wa  matukio mengine 27 ya mauaji unaendelea.
 Aidha, Serikali kwa kutumia Vyombo vyake vya Ulinzi na  Usalama pamoja na kushirikiana na Wananchi, bado inaendelea na juhudi za  kupambana na Wauaji wa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Juhudi hizo ni  pamoja na kufuatilia kazi za Waganga wa Jadi, kuwashawishi Wananchi kuwa  na imani za kiroho, na kuelimisha Jamii ya Watanzania kuondokana na  imani za kishirikina. 
 Ndugu Wananchi, 
 Ili kukabiliana na tatizo hili, Uongozi wa Mikoa yote  umeelekezwa kuhakikisha kuwa Jamii inashirikishwa kikamilifu katika  kulinda maisha ya Wananchi wetu ambao ni Walemavu wa Ngozi. Jeshi la  Polisi nalo linaendelea kuchukua hatua za haraka kila mara linapopata  Taarifa kuhusu hatua zozote za kuhatarisha maisha ya Walemavu wa Ngozi  na Vikongwe. 
 Nimeona nirudie kuyasema haya siku ya leo kwa kuwa pamoja  na hatua kali zinazochukuliwa na Serikali, mauaji haya bado yanaendelea  japo kwa kasi ndogo. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee kwa muda wote.  Watu wenye Ulemavu wa Ngozi wote ni Binadamu na wanayo Haki ya kuishi  kwa amani wakati wote kama Binadamu wengine. Katiba ya Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sehemu ya Tatu Ibara ya 12(1)  na 14 inasema:
 “Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa. Kila Mtu  anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika Jamii Hifadhi ya Maisha  yake kwa mujibu wa Sheria”. 
 Hakuna mahali popote katika Katiba hii ambapo panasema  Walemavu wa Ngozi hawastahili kuishi. Ni kutokana na Msingi huu wa  Kikatiba wa Haki ya kila Mtu kuishi, napenda kusisitiza kuwa Watanzania  wote kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inatokomeza  ukatili na unyama wa aina yoyote wanaofanyiwa Ndugu zetu wenye Ulemavu  wa Ngozi. Napenda kuwaonya Watu wote wanaojihusisha na vitendo viovu vya  ukataji wa Viungo na Wauaji wa Walemavu wa Ngozi popote walipo siku zao  zinahesabika. Ndugu zetu wenye Ulemavu wa Ngozi nawahakikishia Serikali  itashinda Vita hii na mtaishi kwa Uhuru ndani ya Nchi yenu. 
 Nawaomba Watanzania wote na hasa Viongozi wa Dini  kuendelea kuwaelimisha Watanzania juu ya vitendo hivi viovu,  vinavyofanywa na Wauaji hawa. Taasisi zisizo za Kiserikali nao waendelee  kutoa Elimu dhidi ya vitendo vya kikatili kwa Watu wenye Ulemavu wa  Ngozi na kuwasaidia kuendelea na shughuli zao za Kiuchumi na Kijamii  wakiwa huru. Nirudie kauli yangu ya kuwasihi Waganga wa Kienyeji kuacha  kutumika kuchochea ukatili huo. Wasiwadanganye Watu kwani hakuna utajiri  unaopatikana kwa kukata mkono wa Binadamu mwenzako.
 Ndugu Wananchi,
 Serikali kwa kutambua na kuthamini haki za Watu wenye  Ulemavu, hivi karibuni Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha tatizo  hili la Mauaji ya Walemavu wa Ngozi linadhibitiwa kwa kutunga Sheria  ya Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2010. Muswada wa Sheria hii  mpya tayari umepitishwa na Bunge. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa  Kimataifa juu ya Haki za Watu Wenye Ulemavu mnamo mwezi Machi 2007 na  imezindua Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Mwongozo kwa Watu Wenye Ulemavu  mwezi Juni 2008. Tarehe 24 Aprili 2009, Serikali iliridhia Mkataba wa  Kimataifa kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu.
 Juhudi za Asasi  Mbalimbali 
 Ndugu Wananchi,
 Asasi za Watu wenye  Ulemavu zimekuwa zikifanya kazi nzuri kwa kipindi kirefu sasa. Serikali  kwa kutambua umuhimu wa Watu wenye Ulemavu na kwa kushirikiana na Asasi  hizo katika kutoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu; inatenga fedha kama za  Ruzuku kila mwaka kwa lengo la kuvijengea uwezo Vyama vya Watu wenye  Ulemavu. Nimeambiwa kwamba kila Chama cha Watu wenye Ulemavu kinapata  Shilingi Milioni 2.5 kila mwaka kwa madhumuni hayo.  Pamoja na kwamba changamoto kubwa ni kujua idadi halisi ya Asasi hizi na  kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa zinawafikia Walengwa. Yapo  malalamiko kwamba Asasi ni nyingi, lakini haziendani na kiwango cha  huduma zinazotolewa kwa Watu wenye Ulemavu. Aidha, zipo dalili kwamba  baadhi ya Asasi hizi zinatumia nafasi ya Watu wenye Ulema wa Ngozi kwa  kujinufaisha zenyewe. Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu wa kazi  zinazofanywa na Asasi hizi kwenye kuchangia katika jitihada za Serikali  za kutoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu. 
 Kwa vile, masuala ya Watu  wenye Ulemavu ni Mtambuka, jitihada za pamoja ni muhimu ili kufikia  malengo yaliyoainishwa katika miongozo ya Kitaifa na Kimataifa.Ni vizuri  Wizara inayohusika na Asasi hizi kufanyiwa uhakiki ili kubaini zile  ambazo zimetuongezea idadi bila ya kufikisha huduma kwa Walengwa.
 Ndugu Wananchi,
 Hivi sasa, Serikali Kuu  inaendelea kutekeleza Mpango wake wa kugatua Madaraka kwenda katika  ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusogeza huduma za Ustawi wa  Jamii karibu na Wananchi. Hatua hiyo itaziwezesha Halmashauri zote  Nchini kuwa na jukumu kamili la kusimamia na kutekeleza pamoja na mambo  mengine huduma za Watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa  Vyama vya Watu wenye Ulemavu. Vilevile, Serikali imeweza kutenga nafasi  za Watu wenye Ulemavu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  pia kwa Makundi maalum ili kuzingatia Usawa wa Fursa kwa Watu wenye  Ulemavu katika  nafasi za Uongozi. Mbunge wenu Mheshimiwa  Al-Shaymaa John Kwegyir anafanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba  mahitaji maalum ya Watu wenye Ulemavu yanazingatiwa na Serikali katika  kutoa huduma.
 Changamoto
 Ndugu Wananchi,
 Pamoja na juhudi hizo  zilizoonyeshwa na Serikali pamoja na Asasi mbalimbali, wote tunatambua  kuwa safari bado ni ndefu na ambayo inakabiliwa na changamoto  mbalimbali. Kwa mfano, ukosefu wa Elimu na Mafunzo, ukosefu wa Ajira,  Uchumi duni, Unyanyapaa dhidi ya Watu Wenye Ulemavu kutoka kwa Jamii na  kubwa zaidi ni Taarifa za mauaji ya mara kwa mara ya Watu wenye Ulemavu  wa Ngozi.
 Changamoto kubwa ni  kuongeza uhamasishaji kwa Wananchi ili watambue nafasi na haki za Watu  wenye Ulemavu wa Ngozi. Bado uhamasishaji wa ziada unahitajika kwa jamii  yetu na Wadau mbalimbali ili kuwapa Watu Wenye Ulemavu nafasi  wanayostahili katika haki yao ya msingi ya kuishi na kujumuika katika  shughuli mbalimbali za Maendeleo yao, Jamii na Taifa kwa ujumla. Napenda  kutumia nafasi hii kuwaasa Ndugu zetu wenye Ulemavu, kuwa mnalo jukumu  la kuendeleza mshikamano miongoni mwenu na mtumie fursa mbalimbali  mnazozipata kwa manufaa ya jamii yote ya Watu Wenye Ulemavu. Aidha,  mnalo jukumu la kujilinda na kuwalinda wenzenu wakati wowote na mahali  popote. Epukeni kutengeneza mazingira ya kuwa mbali peke yenu hasa  nyakati za usiku. Ni busara kutambua hatari iliyopo mbele yenu na  kuchukua tahadhari mapema. Kwa upande wa Serikali, nawahakikishieni kuwa  Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Usalama kwa kushirikiana na  Wananchi vipo tayari na vimejizatiti kuhakikisha Ulinzi na Usalama wa  Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Nchi kote.
 Upendeleo wa Mikopo
 Ndugu Wananchi,
 Iko hoja iliyotolewa  kwamba Watu wenye Ulemavu wapunguziwe masharti ya Mikopo katika Mabenki.  Tunafahamu kwamba sio rahisi kwa Mabenki na Mashirika yaliyoanzishwa  hapa Nchini kwa ajili ya biashara kutoa kipaumbele cha upendeleo maalum  kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi peke yao. Hata hivyo, Biashara  ya sasa ni huria. Kwa maana hiyo, sio rahisi kuyaagiza Mabenki kuweka  masharti nafuu kwa ajili ya Walemavu wa Ngozi pekee kwa kuwa huduma hii  hutolewa kwa uwiano. Nawashauri ninyi wenyewe muanzishe au mjiunge  kwenye SACCOS ili muweze kupata mikopo kwa ajili ya uzalishaji mali  kujikwamua Kiuchumi. Mkiweza vile vile muendeleze mshikamano miongoni  mwenu na mtumie fursa kujenga SACCOS yenye nguvu, mtaweza kupata fursa  za kupata mitaji kama vile Mabilioni ya JK kwa manufaa yenu na ya Jamii  yote ya Watu Wenye Ulemavu kwa ujumla.
 Kushiriki Uchaguzi Mkuu  2010
 Ndugu Wananchi,
 Mwaka huu ni mwaka wa  Uchaguzi. Tume ya Taifa Uchaguzi imeandaa mipango mizuri yenye lengo la  kuhakikisha kuwa Wananchi wote wanashiriki kikamilifu katika  kujiandikisha na hatimaye kupiga kura ili kuwachagua Viongozi wao.  Aidha, Tume imetoa fursa kwa kila Mwananchi mwenye nia ya kugombea  nafasi yoyote ile kujitokeza na kuweza kugombea. Ni haki ya kila  Mwananchi bila kujali kundi lolote kushiriki kugombea nafasi za Uongozi  Nchini. Napenda kutoa Wito kwa Wananchi wote wakiwemo Watu wenye Ulemavu  wa Ngozi Nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kupitia  Vyama vyao vya Siasa. Kama Kauli mbiu yenu inavyosema “UCHAGUZI  WA SERIKALI, MLEMAVU WA NGOZI ANA HAKI YA KUCHAGUA NA KUCHAGULIWA,  TUJITOKEZE”, mnayo fursa ya kujitokeza kugombea nafasi  mbalimbali za Uongozi kama ilivyo kwa Wananchi wengine. Jitokezeni pia  kwenye zoezi zima la Upigaji kura. Wote mnayo haki ya msingi kushiriki  kikamilifu katika zoezi hili kama ilivyo kwa Watanzania wote.
 Hitimisho
 Ndugu Wananchi,
 Kabla sijamalizia,  napenda kutumia nafasi hii kuzishukuru Taasisi zote za Serikali na  zisizo za Kiserikali zikiwemo Taasisi za Dini ambazo zimeshiriki  kuwasaidia Watu wenye Ulemavu Nchini. Nawashukuru kwa kuona umuhimu wa  kusadia kundi hili muhimu katika Jamii. Wito wangu kwa Taasisi hizi ni  kuwakumbusha na kusisitiza kwamba Watu wenye Ulemavu wanahitaji msaada  mkubwa kutoka kwetu. Tuwasaidie na tushirikiane kuwapatia mahitaji yao  muhimu ikiwa ni pamoja na Elimu, Huduma za Afya na Mazingira mazuri ya  kuwawezesha kuishi bila ya matatizo. Serikali kwa upande wake  itajitahidi kwa uwezo wake kutoa fursa zinazojali mahitaji yao.
 Ndugu Mwenyekiti, Ndugu  Walemavu wa Ngozi, Ndugu Wana Iringa na Wananchi wote,
 Mwisho nitumie nafasi hii  kuwapongeza Viongozi wa Chama cha Walemavu wa Ngozi kwa kutimiza miaka  30 tangu kuanzishwa. Napenda kuwapongeza kwa juhudi kubwa na kazi nzuri  ya kujiendeleza na kukuza Chama chenu hadi hapa mlipofikia. Changamoto  iliyo mbele yenu ni kuhakikisha kuwa Chama chenu kinaendelea kukua na  kupanuka kila pembe ya Tanzania. Hili linawezekana maana Chama chenu  kimeonyesha nia thabiti ya kuboresha huduma zinazotolewa kwa Watu wenye  Ulemavu. Aidha, mmeweza kuielimisha Jamii kuondokana na unyanyapaa na  unyanyasaji kwa Watu wenye Ulemavu kwa ujumla. Mafanikio haya  yanayoonekana, yametokana na Uongozi wenu bora na utulivu wa Wananchama  wenu katika kupanga shughuli zenu ndani ya Chama chenu Nchini. Nawapongeza  Sana!
 Aidha, napenda kusisitiza  kuwa mpango huu wa kuadhimisha Siku ya Walemavu wa Ngozi  Tanzania kila mwaka ni Changamoto ya kupima mafanikio yenu  katika utekelezaji  wa  shughuli  zenu  za  kujiletea  maendeleo. Lengo  ni kujiunga kwa pamoja ndani ya Vyama vyenu na makundi yenu ili kuwa na  mipango ya pamoja itakayowawezesha kutumia fursa zilizopo na  zinazotolewa na Serikali kwa maendeleo yenu. Ni vyema kutambua kuwa Watu  wenye Ulemavu wa Ngozi wana mchango mkubwa katika Jamii hasa  wakiwezeshwa na Binadamu wenzao wasio na Ulemavu huo. Wito wangu kwa  Jamii ya Watanzania ni kuwa Iwape Nafasi Kwani Wanaweza.
 Nawatakia kila la kheri na  mafanikio katika utekelezaji wa shughuli zenu.
 Asanteni sana.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
.jpg) 
 
 
 
.jpg) 
 
 
.jpg) 
 
 
 
.jpg) 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
