I WISH U A MARRY XMASS & HAPPY NEW YEAR 2012

click the word video above 2 watch the clips & cloz 2 back

Thursday, May 6

MKAPA ASHANGAZWA NA NCHI ZA AFRICA KUTEGEMEA MISAADA KUTOKA NCHI ZILIZOENDELEA

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa amesema kuwa anashangazwa kuona bara la Afrika linaendelea kudhani kuwa litaletewa maendeleo na nchi zilizoendelea hivyo kuendelea kuzitegemea.

Akizungumza jana katika Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia kuhusu Afrika kinachomalizika leo jijini Dar es Salam, Mkapa alisema viongozi wengi wa Afrika wanafikiri kuwa ni watu wengine wenye jukumu la kuziletea maendeleo nchi zao.

“Nashangaa sana leo miaka 50 tangu uhuru bado tunategemea wengine watuletee maendeleo? Hili ndio tatizo kubwa ninaloliona kuwa kikwazo cha maendeleo ya Afrika; tunafikiri kuwa ni wengine wenye jukumu la kutuendeleza; tunadhani zipo nchi kwa ajili hiyo hapana; sasa tubadilike. Njia ya kubadilika ni kukubali kubadilika,” alisema Mkapa.

Huku akionyesha msisitizo na kuchukizwa na hali ya kutegemea misaada, Mkapa, ambaye pia ni kamishna wa Tume ya Afrika iliyoanzishwa na aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tonny Blair mwaka 2004, alisema inashangaza zaidi kusikia kiongozi akizungumzia maendeleo anauliza ni wapi au nani atampa fedha na kushindwa hata kufikiria kukopa.

“Inashangaza zaidi, kukuta viongozi wa Afrika wanazungumia maendeleo ya nchi zao, lakini mnauliza ni nani atampa fedha; ni wapi tutapata na wala si kuazima, huu ni ugonjwa,” alisema Mkapa ambaye ni mmoja wa makamishna wa tume hiyo iliyofanya kazi ya kutafiti sababu za Afrika kushindwa kuendelea.

Alisema: “Wakati umefika; simameni kwa miguu yenu; jipangeni na tembeeni kwa miguu yenu, utegemezi ni ugonjwa mkubwa katika Afrika; Tuwe Waafrika”.

Mkapa alitoa mfano wa waziri mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi kuwa anafaa kuigwa katika Afrika kwa kuwa na mawazo, mipango na mikakti inayojitegemea kwa ajili yake, nchi na taifa lake.

“Siwezi kujizuia naomba niseme nampongeza Melesi Zenawi, waziri mkuu wa Ethiopia kwa kuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuwa anafikiri kwa kujitegemea kwa ajili yake na kufanya mambo kwa kujitegemea,” alisema Mkapa.

Rais huyo mstaafu alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa Afrika inategemea kuendelea kwa misaada ya nchi za Ulaya ambazo alisema zinatoa misaada kwa lengo la kuzitawala nchi za Afrika ambazo zimesahau kuwa zilipata uhuru baada ya kuudai kwa nguvu kutoka nchi hizo za Ulaya.

“Tulipambana kudai uhuru kwa kuwa tulijua tukikaa kimya hawatatupa uhuru; tukapiga kelele hata kutumia nguvu ndipo kutapata uhuru.

Sasa itakuwaje hao waliotupa uhuru kwa nguvu watuletee maendeleo? Haiwezekani wao wakoloni wakitusaidia, wanawaza kututawala; tuachane nao tusimame kwa miguu yetu,” alisema Mkapa.

Mkapa anayeongoza pia taasisi yake ya Mkapa Foundation inayojuhusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi, alisema bara hilo pia lina tatizo la kuiga kila jambo kutoka Ulaya, lakini kushindwa kuyafanyia kazi.

Alibainisha kuwa rafiki wa kweli wa maendeleo ya Afrika ni China ambayo alisema haina uhusiano na ukoloni bali wanafikiri juu ya uhusiano, biashara na maendeleo.

“China hawana uhusiano na ukoloni, hawa ni wenzetu, hawafikirii kututawala bali wanataka maendeleo na biashara,” alisema.

Awali Waziri mkuu wa Ethiopia alitaja sababu zinazoifanya Afrika isiendelee kuwa ni pamoja na kukosa miundombinu, rasilimali watu na utawala bora.