I WISH U A MARRY XMASS & HAPPY NEW YEAR 2012

click the word video above 2 watch the clips & cloz 2 back

Wednesday, May 5


MTOTO WA MKULIMA AANZA HOTUBA YAKE KWA WIMBO WA LUCKY DUBE KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA WALEMAVU WA NGOZI TANZANIA TAREHE 04 MEI 2010 VIWANJA VYA GARDEN MJINI IRINGA

Ndugu Wananchi,
Wakati ninapoalikwa kwenye Mikutano, Makongamano, Warsha na Maadhimisho ya Shughuli za Walemavu wa Ngozi kama hii ya leo, huwa ninapata shida sana niseme nini kwa Watanzania na Ulimwengu kwa ujumla. Hii inatokana na kuendelea kuwepo kwa vitendo viovu vya ukatili yakiwemo Mauaji wanayofanyiwa Ndugu zetu, Baba zetu, Mama zetu, Dada zetu na Kaka zetu wenye Ulemavu wa Ngozi ambao tumezoea kuwaita Albino.
Wakati wa Ubaguzi wa Rangi Nchini Afrika Kusini, Mwanamuziki Mashuhuri Barani Afrika – Hayati Lucky Dube aliimba Wimbo unaoitwa – “Different Colours-One People” akiwa na maana ya Rangi Tofauti, Binadamu Mmoja. Moja ya Beti za Wimbo huu unasema:



“Different Colours/one People
Different Colours/one People
Hey you Government
Never try to separate the People
Hey you Politician
Never try to separate the People
They were created in the Image of God
And who are you to separate them
Bible says, He made Man in His Image
But it didn’t say Black or White
Look at me you see BLACK
I look at you I see WHITE
Now is the time to kick that away”

KWA TAFSIRI YA KISWAHILI ISIYO RASMI HAYATI LUCKY DUBE ANAUAMBIA ULIMWENGU KUWA..
“Rangi tofauti – Binadamu Mmoja
Rangi tofauti – Binadamu Mmoja
Nyie Serikali – Msithubutu kubagua Watu
Nyie Wanasiasa –Msithubutu kubagua Watu
Waliumbwa kwa Sura ya Mungu
Nyie ni kina nani muwabague
Biblia inasema: Mungu alimuumba Mtu kwa Mfano wake
Lakini hakusema Mweusi au Mweupe
Niangalie mimi unaniona ni Mweusi
Nikikuangalia naona Mweupe

Nimeona nianze hotuba hii na Wimbo huu wa Hayati Lucky Dube kwa sababu ulikuwa unapinga Ubaguzi wa rangi waliofanyiwa Waafrika Weusi Nchini Afrika ya Kusini wakati wa Utawala wa Makaburu.
Leo hii, Karne ya Sayansi na Teknolojia, Watanzania tunawabagua Walemavu wa Ngozi, tunawakata viungo na kuwaua Ndugu zetu kwa imani za Kishirikina. Hii ni dhambi ambayo hatutasamehewa kwa Mungu. Naomba Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania usimame. Hivi huyu Bwana mbali na yeye kuwa Mweupe na mimi Mweusi tuna tofauti gani nyingine? Mungu amemuumba kama mimi. Kampa viungo vyote kama mimi. Sasa imani za Kijinga kuwa ukipata Kiungo cha Albino utakuwa tajiri zinatoka wapi?
Kama ingekuwa hivyo, kwa nini msiende Nchi za Ulaya na Asia kwa sababu Mabara hayo yana Watu wengi wenye Ngozi Nyeupe ili muwe Matajiri. Nami leo nawaambia Watanzania wote kwamba Mungu ametuumba sote kwa Mfano wake tuachane na imani Potofu za Kishirikina.
Ndugu Wananchi,
Sera ya Taifa ya Walemavu ya mwaka 2004, inaonyesha kuwa, Tanzania kuna Walemavu wa Viungo wapatao takariban 3,456,900. Inasadikiwa kwamba, idadi hii ya Walemavu inaweza ikawa ni kubwa zaidi kwa sasa. Aidha, Takwimu zinazotokana na Sensa Ndogo iliyofanywa kwa haraka haraka mwaka 2007 kutokana na kutokea mauaji ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi zinaonyesha kuwa Tanzania ina Watu wenye Ulemavu wa Ngozi wapatao takriban 8,000. Takwimu hizi ambazo zinahitaji kuhakikiwa zinatoa changamoto kwa Wadau mbalimbali kufanya Sensa itakayotupa hali halisi ya Watu wenye Ulemavu Nchini ili Serikali iweze kupanga mikakati madhubuti katika kuhudumia kundi hili muhimu katika Jamii.
Ndugu Wananchi,
Ni kweli kwamba tunaadhimisha Siku ya Walemavu wa Ngozi Tanzania wakati ambapo bado tunayo Changamoto kubwa ya matukio ya mauaji ya Walemavu hawa Nchini. Tangu Oktoba 2009 hadi sasa, Taarifa tulizonazo ni za Mauaji ya Mlemavu Mmoja (1) wa Ngozi na Watatu (3) waliojeruhiwa. Hata hivyo, pamoja na matukio hayo ya hivi karibuni; hali ya Mauaji ya Walemavu wa Ngozi Nchini yanaonyesha kupungua ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Hali hii ni kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na tatizo hili.
Juhudi za Serikali
Ndugu Wananchi,
Moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuitisha Kura ya Maoni kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya Mapambano dhidi ya Vitendo vya Ukatili kwa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Serikali iliwataka Wananchi kutaja Watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na Mauaji au kukata Viungo vya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi, wawataje Waganga wa Jadi wanaohusika, Wauaji, Wauzaji wa Viungo na Wafanyabiashara wanaotumia Viungo hivyo.
Zoezi la Kura ya Maoni lilifanyika kwa Mikoa yote Tanzania Bara mwezi Machi 2009. Jumla ya Watu 97,736 walipigiwa Kura kuwa wanahusika na makosa mbalimbali yakiwemo ya Mauaji ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Upelelezi wa kina unaendelea kuhusu Watuhumiwa na wale wote ambao ushahidi unapatikana wanafikishwa Mahakamani. Hadi sasa, Watu 3,217 wamefikishwa katika Vituo vya Polisi, Watu 295 wamefikishwa Mahakamani na Watu 106 wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwemo ya Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Kati ya kesi zilizofikishwa Mahakamani, 11 ni za mauaji ya Walemavu wa Ngozi. Kesi tatu zimetolewa hukumu na Watuhumiwa Wanane (8) wamehukumiwa kifo. Upelelezi wa matukio mengine 27 ya mauaji unaendelea.
Aidha, Serikali kwa kutumia Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama pamoja na kushirikiana na Wananchi, bado inaendelea na juhudi za kupambana na Wauaji wa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Juhudi hizo ni pamoja na kufuatilia kazi za Waganga wa Jadi, kuwashawishi Wananchi kuwa na imani za kiroho, na kuelimisha Jamii ya Watanzania kuondokana na imani za kishirikina.
Ndugu Wananchi,
Ili kukabiliana na tatizo hili, Uongozi wa Mikoa yote umeelekezwa kuhakikisha kuwa Jamii inashirikishwa kikamilifu katika kulinda maisha ya Wananchi wetu ambao ni Walemavu wa Ngozi. Jeshi la Polisi nalo linaendelea kuchukua hatua za haraka kila mara linapopata Taarifa kuhusu hatua zozote za kuhatarisha maisha ya Walemavu wa Ngozi na Vikongwe.
Nimeona nirudie kuyasema haya siku ya leo kwa kuwa pamoja na hatua kali zinazochukuliwa na Serikali, mauaji haya bado yanaendelea japo kwa kasi ndogo. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee kwa muda wote. Watu wenye Ulemavu wa Ngozi wote ni Binadamu na wanayo Haki ya kuishi kwa amani wakati wote kama Binadamu wengine. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sehemu ya Tatu Ibara ya 12(1) na 14 inasema:
“Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa. Kila Mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika Jamii Hifadhi ya Maisha yake kwa mujibu wa Sheria”.
Hakuna mahali popote katika Katiba hii ambapo panasema Walemavu wa Ngozi hawastahili kuishi. Ni kutokana na Msingi huu wa Kikatiba wa Haki ya kila Mtu kuishi, napenda kusisitiza kuwa Watanzania wote kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inatokomeza ukatili na unyama wa aina yoyote wanaofanyiwa Ndugu zetu wenye Ulemavu wa Ngozi. Napenda kuwaonya Watu wote wanaojihusisha na vitendo viovu vya ukataji wa Viungo na Wauaji wa Walemavu wa Ngozi popote walipo siku zao zinahesabika. Ndugu zetu wenye Ulemavu wa Ngozi nawahakikishia Serikali itashinda Vita hii na mtaishi kwa Uhuru ndani ya Nchi yenu.
Nawaomba Watanzania wote na hasa Viongozi wa Dini kuendelea kuwaelimisha Watanzania juu ya vitendo hivi viovu, vinavyofanywa na Wauaji hawa. Taasisi zisizo za Kiserikali nao waendelee kutoa Elimu dhidi ya vitendo vya kikatili kwa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi na kuwasaidia kuendelea na shughuli zao za Kiuchumi na Kijamii wakiwa huru. Nirudie kauli yangu ya kuwasihi Waganga wa Kienyeji kuacha kutumika kuchochea ukatili huo. Wasiwadanganye Watu kwani hakuna utajiri unaopatikana kwa kukata mkono wa Binadamu mwenzako.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kutambua na kuthamini haki za Watu wenye Ulemavu, hivi karibuni Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha tatizo hili la Mauaji ya Walemavu wa Ngozi linadhibitiwa kwa kutunga Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2010. Muswada wa Sheria hii mpya tayari umepitishwa na Bunge. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Watu Wenye Ulemavu mnamo mwezi Machi 2007 na imezindua Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Mwongozo kwa Watu Wenye Ulemavu mwezi Juni 2008. Tarehe 24 Aprili 2009, Serikali iliridhia Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu.
Juhudi za Asasi Mbalimbali
Ndugu Wananchi,
Asasi za Watu wenye Ulemavu zimekuwa zikifanya kazi nzuri kwa kipindi kirefu sasa. Serikali kwa kutambua umuhimu wa Watu wenye Ulemavu na kwa kushirikiana na Asasi hizo katika kutoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu; inatenga fedha kama za Ruzuku kila mwaka kwa lengo la kuvijengea uwezo Vyama vya Watu wenye Ulemavu. Nimeambiwa kwamba kila Chama cha Watu wenye Ulemavu kinapata Shilingi Milioni 2.5 kila mwaka kwa madhumuni hayo. Pamoja na kwamba changamoto kubwa ni kujua idadi halisi ya Asasi hizi na kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa zinawafikia Walengwa. Yapo malalamiko kwamba Asasi ni nyingi, lakini haziendani na kiwango cha huduma zinazotolewa kwa Watu wenye Ulemavu. Aidha, zipo dalili kwamba baadhi ya Asasi hizi zinatumia nafasi ya Watu wenye Ulema wa Ngozi kwa kujinufaisha zenyewe. Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu wa kazi zinazofanywa na Asasi hizi kwenye kuchangia katika jitihada za Serikali za kutoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu.
Kwa vile, masuala ya Watu wenye Ulemavu ni Mtambuka, jitihada za pamoja ni muhimu ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika miongozo ya Kitaifa na Kimataifa.Ni vizuri Wizara inayohusika na Asasi hizi kufanyiwa uhakiki ili kubaini zile ambazo zimetuongezea idadi bila ya kufikisha huduma kwa Walengwa.
Ndugu Wananchi,
Hivi sasa, Serikali Kuu inaendelea kutekeleza Mpango wake wa kugatua Madaraka kwenda katika ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusogeza huduma za Ustawi wa Jamii karibu na Wananchi. Hatua hiyo itaziwezesha Halmashauri zote Nchini kuwa na jukumu kamili la kusimamia na kutekeleza pamoja na mambo mengine huduma za Watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu. Vilevile, Serikali imeweza kutenga nafasi za Watu wenye Ulemavu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa Makundi maalum ili kuzingatia Usawa wa Fursa kwa Watu wenye Ulemavu katika nafasi za Uongozi. Mbunge wenu Mheshimiwa Al-Shaymaa John Kwegyir anafanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba mahitaji maalum ya Watu wenye Ulemavu yanazingatiwa na Serikali katika kutoa huduma.
Changamoto
Ndugu Wananchi,
Pamoja na juhudi hizo zilizoonyeshwa na Serikali pamoja na Asasi mbalimbali, wote tunatambua kuwa safari bado ni ndefu na ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Kwa mfano, ukosefu wa Elimu na Mafunzo, ukosefu wa Ajira, Uchumi duni, Unyanyapaa dhidi ya Watu Wenye Ulemavu kutoka kwa Jamii na kubwa zaidi ni Taarifa za mauaji ya mara kwa mara ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi.
Changamoto kubwa ni kuongeza uhamasishaji kwa Wananchi ili watambue nafasi na haki za Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Bado uhamasishaji wa ziada unahitajika kwa jamii yetu na Wadau mbalimbali ili kuwapa Watu Wenye Ulemavu nafasi wanayostahili katika haki yao ya msingi ya kuishi na kujumuika katika shughuli mbalimbali za Maendeleo yao, Jamii na Taifa kwa ujumla. Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa Ndugu zetu wenye Ulemavu, kuwa mnalo jukumu la kuendeleza mshikamano miongoni mwenu na mtumie fursa mbalimbali mnazozipata kwa manufaa ya jamii yote ya Watu Wenye Ulemavu. Aidha, mnalo jukumu la kujilinda na kuwalinda wenzenu wakati wowote na mahali popote. Epukeni kutengeneza mazingira ya kuwa mbali peke yenu hasa nyakati za usiku. Ni busara kutambua hatari iliyopo mbele yenu na kuchukua tahadhari mapema. Kwa upande wa Serikali, nawahakikishieni kuwa Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Usalama kwa kushirikiana na Wananchi vipo tayari na vimejizatiti kuhakikisha Ulinzi na Usalama wa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Nchi kote.
Upendeleo wa Mikopo
Ndugu Wananchi,
Iko hoja iliyotolewa kwamba Watu wenye Ulemavu wapunguziwe masharti ya Mikopo katika Mabenki. Tunafahamu kwamba sio rahisi kwa Mabenki na Mashirika yaliyoanzishwa hapa Nchini kwa ajili ya biashara kutoa kipaumbele cha upendeleo maalum kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi peke yao. Hata hivyo, Biashara ya sasa ni huria. Kwa maana hiyo, sio rahisi kuyaagiza Mabenki kuweka masharti nafuu kwa ajili ya Walemavu wa Ngozi pekee kwa kuwa huduma hii hutolewa kwa uwiano. Nawashauri ninyi wenyewe muanzishe au mjiunge kwenye SACCOS ili muweze kupata mikopo kwa ajili ya uzalishaji mali kujikwamua Kiuchumi. Mkiweza vile vile muendeleze mshikamano miongoni mwenu na mtumie fursa kujenga SACCOS yenye nguvu, mtaweza kupata fursa za kupata mitaji kama vile Mabilioni ya JK kwa manufaa yenu na ya Jamii yote ya Watu Wenye Ulemavu kwa ujumla.
Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2010
Ndugu Wananchi,
Mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi. Tume ya Taifa Uchaguzi imeandaa mipango mizuri yenye lengo la kuhakikisha kuwa Wananchi wote wanashiriki kikamilifu katika kujiandikisha na hatimaye kupiga kura ili kuwachagua Viongozi wao. Aidha, Tume imetoa fursa kwa kila Mwananchi mwenye nia ya kugombea nafasi yoyote ile kujitokeza na kuweza kugombea. Ni haki ya kila Mwananchi bila kujali kundi lolote kushiriki kugombea nafasi za Uongozi Nchini. Napenda kutoa Wito kwa Wananchi wote wakiwemo Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kupitia Vyama vyao vya Siasa. Kama Kauli mbiu yenu inavyosema “UCHAGUZI WA SERIKALI, MLEMAVU WA NGOZI ANA HAKI YA KUCHAGUA NA KUCHAGULIWA, TUJITOKEZE”, mnayo fursa ya kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi kama ilivyo kwa Wananchi wengine. Jitokezeni pia kwenye zoezi zima la Upigaji kura. Wote mnayo haki ya msingi kushiriki kikamilifu katika zoezi hili kama ilivyo kwa Watanzania wote.
Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Kabla sijamalizia, napenda kutumia nafasi hii kuzishukuru Taasisi zote za Serikali na zisizo za Kiserikali zikiwemo Taasisi za Dini ambazo zimeshiriki kuwasaidia Watu wenye Ulemavu Nchini. Nawashukuru kwa kuona umuhimu wa kusadia kundi hili muhimu katika Jamii. Wito wangu kwa Taasisi hizi ni kuwakumbusha na kusisitiza kwamba Watu wenye Ulemavu wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwetu. Tuwasaidie na tushirikiane kuwapatia mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na Elimu, Huduma za Afya na Mazingira mazuri ya kuwawezesha kuishi bila ya matatizo. Serikali kwa upande wake itajitahidi kwa uwezo wake kutoa fursa zinazojali mahitaji yao.
Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Walemavu wa Ngozi, Ndugu Wana Iringa na Wananchi wote,
Mwisho nitumie nafasi hii kuwapongeza Viongozi wa Chama cha Walemavu wa Ngozi kwa kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa. Napenda kuwapongeza kwa juhudi kubwa na kazi nzuri ya kujiendeleza na kukuza Chama chenu hadi hapa mlipofikia. Changamoto iliyo mbele yenu ni kuhakikisha kuwa Chama chenu kinaendelea kukua na kupanuka kila pembe ya Tanzania. Hili linawezekana maana Chama chenu kimeonyesha nia thabiti ya kuboresha huduma zinazotolewa kwa Watu wenye Ulemavu. Aidha, mmeweza kuielimisha Jamii kuondokana na unyanyapaa na unyanyasaji kwa Watu wenye Ulemavu kwa ujumla. Mafanikio haya yanayoonekana, yametokana na Uongozi wenu bora na utulivu wa Wananchama wenu katika kupanga shughuli zenu ndani ya Chama chenu Nchini. Nawapongeza Sana!
Aidha, napenda kusisitiza kuwa mpango huu wa kuadhimisha Siku ya Walemavu wa Ngozi Tanzania kila mwaka ni Changamoto ya kupima mafanikio yenu katika utekelezaji wa shughuli zenu za kujiletea maendeleo. Lengo ni kujiunga kwa pamoja ndani ya Vyama vyenu na makundi yenu ili kuwa na mipango ya pamoja itakayowawezesha kutumia fursa zilizopo na zinazotolewa na Serikali kwa maendeleo yenu. Ni vyema kutambua kuwa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi wana mchango mkubwa katika Jamii hasa wakiwezeshwa na Binadamu wenzao wasio na Ulemavu huo. Wito wangu kwa Jamii ya Watanzania ni kuwa Iwape Nafasi Kwani Wanaweza.
Nawatakia kila la kheri na mafanikio katika utekelezaji wa shughuli zenu.
Asanteni sana.