Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto ambaye amekitupia lawama Chama Cha Mapinduzi kwa kushindwa kupunguza umaskini nchini
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ameishambulia CCM kwa kushindwa kuondoa umasikini nchini katika kipindi cha miaka minne iliyopita, licha ya serikali yake kuidhinishiwa bajeti inayoomba kila mwaka.Akichangia hoja ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2010/11 bungeni jana, alisema haijalenga (bajeti hiyo) katika shughuli za maendeleo, badala yake imejikita zaidi katika kuwashibisha watu wenye uwezo na kuzidi kuangamiza walalahoi. “Hii ni bajeti mbaya. Ni kwa ajili ya tumbo. Ina faida zaidi kwa wenye uwezo,” alisema Zitto. Alisema kutokana na ubaya wa bajeti hiyo, watakaoumia zaidi ni walalahoi wanaofikia 13 milioni nchini ambao wanaishi kwa dola moja ya Marekani (Sh 1,400) kwa siku. “Ni bajeti ambayo ina faida zaidi kwa wenye uwezo,” alisema Zitto akichambua kuwa imeshindwa kujitosheleza kutokana na mapato ya ndani. Ili kuendesha nchi kwa bajeti hiyo, Zitto alisema: “Itabidi serikali ikope kwa wahisani kwa ajili ya kulipa mishahara wafanyakazi, kulipa posho na kununua mafuta kwa ajili ya magari”. Akionekana kuwa makini na aliyepangilia hoja zake zilizotiwa na nguvu ya takwimu, Zitto alikigeukia CCM na kusema chama hicho kinapaswa kubeba lawama zote kwa sababu kimeshindwa kutekeleza ahadi zake kulingana na Ilani yake ya mwaka 2005. Kuhusu Chuo Kikuu Dodoma Zitto alidai; "Hilo halipo katika ahadi za CCM, kama yupo mbunge wa CCM asimame aje aonyeshe ni wapi Ilani ya CCM ilipotoa ahadi itajenga Udom, hakuna, hakuna, ‘nachallenge’; kama yupo anayeweza kuonysha aje. Ujenzi wa Udom ni wazo na ahadi ya Chadema ya mwaka 1992". Maneno hayo yaliyomwinua Mbunge wa Ukerewe, Dk Getrude Mongella (CCM) na kuombna mwongozo wa Spika. "Mwongozo wa Spika. Hivi ni utaratibu mzuri kuwaambia Watanzania kupitia Bunge kwamba, CCM ilidanganya", alihoji Mongella baada ya kumyamazisha Zitto kwa kuomba mwongozo wa Spika. Hoja ya Mongella iliungwa mkono na Naibu Spika, Anna Makinda aliyeongoza kikao hicho jana asubuhi. "Upo sahihi Mheshimiwa Mongella, lakinin lazima tukubali kuwa katika wakati huu, ndio wakati hayo yatatokea tu", alisema Makinda. Akichangia hotuba hiyo, Zitto alitumia maneno makali akisema bajeti hiyo ni sawa na barua ndefu ya CCM kutaka kujinyonga kwa kuwa ni ya kuchumia tumbo. " Toka serikali iingie madarakani kwa miaka minne iliyopita Bunge limeidhinisha zaidi ya Sh26trilioni kama bajeti, kutoka 2006/2007 mpaka mwaka 2009/2010. Leo na mpaka Jumatatu tunajadili, na kwa wingi wa wabunge wa CCM kwa vyovyote vile watapewa cheki nyingine ya Sh11trilioni pia. “Kwa ujumla katika miaka mitano, tutakuwa tumewapa jumla ya Sh37trilioni kwa ajili ya kuleta maendeleo, laikini katika miaka minne iliyopita jumla ya Watanzania 1.6 milioni wamekuwa maskini", alisema Zitto. Aliongeza kuwa hadi wakati huu idadi ya watu maskini nchini imefikia 13milioni ambao wanaoishi chini ya dila moja kwa siku, lakini bajeti hiyo ikikaa kimya bila kueleza jinsi itakavyowaondoa katika kadhia hiyo. Alisema bajeti hiyo inatoa faida zaidi kwa watu wenye uwezo ikiwaacha maskini bila ufumbuzi na kwamba, matumizi ya ndani yana pengo la Sh1.8 trilioni, hivyo katika kila Sh100 inayotumiwa, serikali inakopa kiasi cha Sh23. Akichangia bajeti hiyo, DkMongella aliwatuhumu wakurugenzi wa maendeleo wa wilaya kuwa kikwazo cha maendeleo kwa kukosa ubunifu. Alifafanua: “Kupitia Mkukuta (Mpango wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania) unaonyesha kwamba utapunguza umasikini nchini kwa kati ya asilimia nane hadi kumi.” Akichangia hotuba hiyo Mbunge wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga aligusia zaidi sekta ya miundombinu hasa bandari na reli akisema kuwa ipo haja kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuliponyesha Shirika la Reli nchini (TRL), alilosema ni sawa na mgonjwa aliyelazwa katika chumba cha wangongwa mahututi. "Bandari zikitumika vizuri zitainua uchumi, tatizo miundombinu yetu, reli, TRL ni gonjwa, lipo ICU, ipo haja ya kuliponyesha haraka. Shirika halina injini, mabehewa mabovu, bado halijaanza kazi licha ya kipande cha reli kilichoharibika Kilosa kutengenezwa. Halina fedha hata za kununulia mafuta. Serikali itenge fedha kulinusuru shirika hili". Alisema Kaboyonga. Wabunge wengine waliochangia mjadala wa hotuba hiyo ya bajeti hadi jana mchana ni pamoja na, Abdalah Mtutura, Juma Killimbah, Mgana Msindai na Chrisant Mzindakaya aliyesema takwimu za Benki ya Dunia (WB)za mwaka 2007 zinaonyesha kuwa asilimia 89 ya Watanzania ni maskini na kuongeza kuwa wengi wa Watanzania ni wavivu. Wengine ni Athuman Janguo na Herbert Mntangi, Khadija Saleh Ngozi ambao walionyesha wasiwasi kuhusu kampuni kubwa za madini kupewa misamaha ya kodi katika mafuta ya kuendeshea mitambo. Mjadala huo wa bajeti unaendelea leo na Jumatatu jioni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo atahitimisha kwa kujibu hoja za wabunge.