*Nusu ya wanafunzi waambulia daraja 0
*Wasichana hawashikiki, wavulana hoi
*Katika kumi bora wachukua nafasi nane
*Shule za Dar, K`njaro, Moro, Mbeya juu
Matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne yaliyotangazwa jana yanaonyesha kwamba wasichana wamewapiku kwa mbali wavulana, wakikalia nafasi nane kati ya kumi bora, huku nusu ya watahiniwa wote wakiambulia daraja sifuri.
Katika matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako, jumla ya watahiniwa 352,840 waliofanya mtihani huo ni 177,021 tu waliofaulu.
Matokeo ya mtihani huo uliofanyika mwaka Oktoba mwaka jana pia yanaonyesha kuwa watahiniwa wanne wamefutiwa matokeo kwa kuandika matusi mazito kwenye karatasi za kujaza majibu.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa shule binafsi 10 ndizo zinazoongoza katika kundi la shule kumi bora kitaifa zilizofanya vizuri.
Dk. Ndalichako alisema watahiniwa wa shule waliosajiliwa ni 363,589, lakini waliofanya mitihani ni 352,840, waliofaulu wakiwa ni 177,021 sawa na asilimia 50.4.
Katika kundi la waliofaulu, wasichana ni 69,996 sawa na asilimia 43.3 na wavulana ni 107,025 sawa na asilimia 56.
Alisema watahiniwa binafsi waliosajiliwa walikuwa 94,525 na kati ya hao waliofaulu walikuwa 46,064 sawa na asilimia 52.
Katika ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, Dk. Ndalichako alisema 40, 388 sawa na asilimia 11.5 wamefaulu katika madaraja ya I hadi III na kwamba wasichana waliofaulu katika madaraja hayo ni 12,583 na wavulana ni 27,805.
Alisema jumla ya wanafunzi waliopata daraja 0 ni 174,193 ambao ni karibu nusu ya wanafunzi wote waliofanya mitihani hiyo.
Jedwali la matokeo linaonyesha kuwa wavulana waliopata darala la kwanza I ni 3,874 na wasichana ni 1,489, daraja la II wavulana ni 7,003 na wasichana ni 2,939, daraja la III wavulana ni 16,928, wasichana ni 8,155 na daraja la IV wavulana ni 79,220 na wasichana ni 57,413.
SHULE KALI 10
Alitaja shule 10 zilizoongoza kitaifa na mikoa yake katika mabano kuwa ni Uru Seminary (Kilimanjaro), Marian Girls (Pwani), St Francis Girls (Mbeya), Canossa (Dar es Salaam), Msolwa (Morogoro), Feza Boys (Dar es Salaam), St Mary Goreti (Kilimanjaro), Abbey (Mtwara), St Joseph’s Sem Iterarambogo (Kigoma) na Barbro-Johanson (Dar es Salaam).
WANAFUNZI WAKALI 10
Aliwataja wanafunzi bora 10 kitaifa ambao walifanya vizuri kuliko wote na shule zao katika mabano kuwa ni Lucylight Mallya na Maria-Dorin Shayo (Marian Girls).
Wengine ni Sherryen Cessar (Barbro-Johanson), Diana Abel Matabwa (St Francis Girls), Neema Joey Kafwimi (St Francis) na Beatrice Issara (St Mary Goreti).
Wengine ni Johnston Dedani (Ilboru) mkoani Arusha, Samwel M. Emmanuel (Moshi Tech), Bertha Sanga (Marian Girls) na Bernadetha Kalluvya (St Francis Girls).
Aliwataja wavulana kumi walioongoza kitaifa kuwa ni Johnston Dedani (Ilboru), Samwel Emmanuel (Moshi Tech), Jimoku Salum (Shinyanga Sekondari), Amaniel Barabara (Arusha Day), Aswile Mwambembe (Kibaha), James Mwitondi (Loyola), Gasper Mung’ong’o (Loyola), Yohane Kihaga (Don Bosco Seminary (Iringa) na Tonny Tarimo wa (Msolwa, Morogoro).
Dk. Ndalichako alisema Necta inashikilia matokeo ya watahiniwa 1,448 waliofanya mitihani bila kulipa ada hadi hapo watakapolipa pamoja na faini katika kipindi cha miaka miwili.
Alisema watahiniwa 311 wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu wa aina mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Dk. Ndalichako aliwaonya wanafunzi wa kidato cha sita ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwezi ujao kuacha kuandika matusi kwenye mitihani yao hata kama imewashinda.
“Nawaomba kidato cha sita wasifanya mchezo huu kabisa, maana inaonekana kama inaanza kuwa mazoea. Mwaka jana kulikuwa na mwanafunzi mmoja aliyeandika matusi kwenye karatasi ya majibu mwaka huu idadi imeongezeka na kuwa wanne,” alisema Dk. Ndalichako.
nibofye kusoma matokeo haya...
http://www.necta.go.tz/matokeo2010/csee2010/olevel.htm