Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Askofu mpya wa Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Tarime Dr. Raphael Mwita na Askofu mkuu Valen SAA chache tu baada ya msafara wa Rais Jakaya Kikwete, kuingia katika Kanisa a Anglikana, ili kuhudhuria sherehe za kuwekwa wakfu Askofu, askari polisi wa kike WP Suzana, amejiua kwa kujipiga risasi baada ya kuwekwa mahabusu kwa kosa la kuupoteza njia, msafara wa Rais.
Habari zilisema tukio hilo lililogeuka kuwa gumzo katika mji huo, lilitokea saa 8 mchana wa jana, katika Kituo cha Polisi Tarime, muda mfupi baada ya askari huyo kuwekwa chini ya ulinzi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Dk Charles Samson, alikiri kuupokea mwili wa askari huyo na kwamba alijipiga risasi upande wa kushoto wa kifua.
Kwa mujibu wa Mganga huyo, risasi hiyo ilipenya na kutokea nyuma ya bega.
"Ni kweli amejiua kwa kujipiga risasi ambayo imetokea nyuma ya bega. Kwa ufupi ni kwamba eneo hilo ni sehemu ya moyo, nimemfanyia uchunguzi wa awali na
kuthibitisha kuwa amekufa,"alisema.
Alisema taarifa kuhusu tukio hilo alizipata akiwa katika msafara wa Rais na kwamba alipokwenda kumfanyia uchunguzi marehemu, alibaini kuwa alikata roho muda mfupi,baada ya kujipiga risasi.
"Kitaalam kilichosabaisha kifo ni risasi maana nimefanya uchunguzi na kubaini, nasubiri uchunguzi mkubwa tukiwa na polisi ili tuwakabidhi maiti kwa ajili ya hatua nyingine,"alisema kwa masikitiko.
"Sijui nini kimempelekea kujiua maana huo ni uamuzi mzito sana aliochukua," alisisitiza Mganga mkuu.
Kwa upande wake, mhudumu wa chumba cha maiti katika hospitali hiyo, Samweli Malindi, alisema marehemu alifikishwa katika katika chumba hicho kwa kutumia gari la polisi.
"Walisema amejiua kwa sababu ya kuongoza vibaya msafara wa Rais na kuwekwa mahabusu," alisema.
Chanzo kimoja cha uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo, kililiambia
gazeti hili kuwa kiini cha askari huyo kujiua ni kuwekwa mahabusu huku akitishiwa kuchukuliwa hatua kali zaidi.
Chanzo hicho kilisema msafara wa Rais ulitakiwa kuingia kwa mkuu wa wilaya, kabla ya kwenda kanisani, lakini yeye aliruhusu magari kwenda moja kwa moja na gari la Rais likielekea kwa mkuu wa wilaya, jambo lililosababisha safara ukagawanyika na baadaye kulazimika kurudi.
"Kitendo hicho kiliwachukiza viongozi na kuamuru kukamatwa na kuwekwa
mahabusu kwa askari huyo. Wakati akiwa mapokezi ghafla alichukua bunduki aina ya SMG na kujimiminia risasi tatu na kukata roho papo hapo," kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilidai kuwa askari huyo ni miongoni mwa askari polisi waliotoka chuoni hivi karibuni na kwa hiyo si mzoefu.
Chanzo hicho kilisema katika hali ya kawaida viongozi walipaswa kumsaidia kwa kutumia lugha ambayo vinginevyo isingemfanya ajisikie vibaya na kuchukua uamuzi huo. Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mwananchi walisema hayo ni matatizo ya matumizi ya nguvu ndani ya jeshi.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalumu ya Polisi ya Tarime/Rorya, Constantine Masawe,alisema alikuwa nje ya ofisi."Niko Dar es Salaam na wala sikuwa na taarifa, amejiua kwa nini, maana sijaambiwa,"alisema.
Rais Kikwete, alikuwa amekwenda Tarime kuhudhuria kuwekwa wakfu kwa Askofu Dk Mwita Akiri.